WATU 11 WAKIWEMO POLISI WANANE WAUAWA TURKANA.

Hali ya Taharuki ingali imetanda katika eneo la Kamuge Turkana Mashariki, baada ya wezi wa mifugo kushambulia gari la polisi  lililokuwa limebeba maafisa 8  wa usalama, Chifu wa Napeitom  na mwanamke mmoja  na kuwaua papo hapo huku wengine watatu wakijeruhiwa.

Kamanda wa Polisi Turkana Samuel Ndanyi, amesema kisa hiki kilitokea baada ya wezi wa mifugo kuvamia Kijiji Cha Namariat alfajiri ya Jumamosi na kutoweka na mifugo ambapo maafisa wa usalama kutoka Lokori walijipanga kuelekea upande wa mbele kuzuia wezi hao kwa lengo la kurejesha mifugo na hapo ndipo wakatumbukia kwenye mtego wa majambazi hao..

Majeruhi walikimbizwa katika hospitali ya rufaa ya Lodwar huku Ndege ya Polisi ikielekea eneo la mkasa na kubeba miili ya maafisa hao 8 wa usalama na kuwapeleka jijini Nairobi.

Viongozi wa Turkana  wakiongozwa na seneta wa kaunti hiyo James Lomenen pamoja na gavana wa Jeremiah lomorukai wameitaka serikali ifidie familia zilizoathirika.

“Polisi ambao wamekuja kuokoa watu tena wanauwa. Sasa askari wakiuawa wananchi watahakikishiwa aje usalama wao. Sasa kile ninauliza ni watu wangapi serikali inataka wauawe Turkana ndipo wachukue hatua?” Walisema.

Waliongeza kuwa, “watu wa Turkana wanapasa kutendewa haki. Tumepoteza idadi kubwa ya wakazi kutokana na wizi wa mifugo. Tumepoteza maafisa wengi wa usalama ambao walijitolea kulinda maisha ya wakazi. Tunahisi tunafaa kutendewa haki na serikali ya Kenya.”

Wakati uo huo rais William Ruto aliwahakikishia wakenya kwamba uongozi wake utakabili kikamilifu swala la wizi wa mifugo huku akitoa wito kwa wakenya kuwaombea maafisa wa usalama nchini wanapotekeleza majukumu yao.

“Tuviombee vikosi vyetu vya usalama ili vitekeleze majukumu yao vyema. Katika majuma kadhaa yaliyopita nilitoa mamlaka kwa idara ya polisi kuwa na bajeti yake ili wasisubiri tena afisi ya rais.” Alisema.

[wp_radio_player]