WATOTO WAWILI WAUAWA HUKU ZAIDI YA MIFUGO 100 WAKIIBWA KATIKA UVAMIZI WA HIVI PUNDE TURKWEL.

Viongozi katika kaunti ya Pokot magharibi wamekashifu vikali uvamizi uliotekelezwa na wahalifu wanaoaminika kutoka kaunti jirani katika kijiji cha Kamurio eneo la Turkwel ambapo waliiba zaidi ya mifugo 100 huku watoto wawili wakiuliwa na wavamizi hao.

Wakiongozwa na mwakilishi wadi mteule Marshono Cheruto, viongozi hao walisema, inasikitisha kuona kwamba visa vya mauaji yanayosababishwa na wezi wa mifugo vimeendelea kushuhudiwa eneo hilo licha ya kuwepo na oparesheni ya kiusalama.

Cheruto aidha aliwasuta wavamizi hao kwa kuwalenga watoto akisema huenda wahalifu hao wanatumia kisingizio cha wizi wa mifugo kutimiza malengo yao ya kutekeleza mauaji dhidi ya wakazi kutoka jamii ya pokot.

”Ninashutumu sana mauaji ambayo yamefanyika huko Turkwel ambapo watoto wawili walipigwa risasi na majambazi kutoka kaunti jirani. Ni kwa nini watoto wadogo wanapigwa risasi? Naona nia ya  hawa watu ni kuwaua tu wakazi wa jamii ya Pokot kwa kusingizia wizi wa mifugo.” Alisema Cheruto.

Aliwataka viongozi kutoka kaunti ya Pokot magharibi na kaunti jirani ya Turkana kushirikliana na serikali kuu katika kutafuta mbinu za kuhakikisha kwamba hali ya usalama inadumishwa eneo la Turkwel na kuwapa wakazi mazingira bora ya kutekeleza shughuli zao.

“Gavana wa kaunti ya Turkana, wabunge na waakilishi wadi wakae chini, sisi huku pia tukae chini ili tuzungumzie maswala haya ya amani. Tushirikiane na serikali kuhakikisha kwamba wananchi wanaishi kwa amani na kutekeleza shughuli zao.” Alisema.