WATOTO WANNE WANASWA BAADA YA KUKEKETWA KACHELIBA POKOT MAGHARIBI.
Licha ya juhudi na mikakati iliyowekwa na serikali pamoja na mashirika mbali mbali katika kaunti hii ya Pokot magharibi kukabili tamaduni ya ukeketaji wa watoto wa kike, visa hivi vimeendelea kuripotiwa katika kaunti hii.
Hii ni baada ya wasichana wanne kunaswa na maafisa wa polisi wa kituo cha kacheliba wakiwa tayari wamekeketwa na kufichwa katika sehemu moja eneo la Koropamenyon kwenye lokesheni ya suam eneo bunge la Kacheliba.
Kisa hicho kiliripotiwa na chifu wa eneo hilo baada ya kupata fununu za kutekelezwa kitendo hicho kilichoharamishwa nchini kabla ya maafisa wa polisi kuanzisha oparesheni na kuwanasa nne hao huku mmoja miongoni mwao akinusuriwa kabla ya kukeketwa.
“Hii leo tumepata ripoti kwamba watoto wanne wasichana wamekeketwa na kufichwa sehemu fulani katika kijiji cha Koropamenyon. Lakini nampongeza chifu wa eneo hili kwa ripoti ambayo alitoa kwa polisi kuhusiana na kisa hicho. Ni wanafunzi wadogo sana ila sasa wako mikononi mwa polisi.” Alisema kiongozi wa kikundi kimoja cha vijana eneo la Kacheliba Joseph Sarich.
Ni kisa ambacho kimeshutumiwa vikali na wakazi wa eneo hilo ambao wamelaumu likizo ndefu ambayo wanafunzi wamesalia nyumbani baada ya shule kufungwa mwezi novemba mwaka jana wakitoa wito kwa jamii kujitenga na tamaduni hiyo iliyopitwa na wakati.
“Nasikitika sana kwa jambo hili. Tamaduni kama hizi zilipitwa na wakati. Sasa ni wakati ambapo tunafaa kuangazia maswala ambayo yana faida wala si kuendeleza tena ukeketaji. Jamii inafaa kujitenga na tabia hii na kuangazia maswala yenye umuhimu.” Walisema wakazi.
Kisa hicho kilithibitishwa na OCS wa kituo cha polisi cha Kacheliba Tom Nyanaro ambaye aidha alisema kuwa wazazi wa watoto waliokeketwa wanazuiliwa katika kituo hicho cha polisi na watafikishwa mahakamani kujibu mashitaka ya kuendeleza tamaduni hiyo iliyoharamishwa.