WATAHINIWA WA MITIHANI YA KITAIFA POKOT MAGHARIBI WAHAKIKISHIWA USALAMA WA KUTOSHA KATIKA KIPINDI HICHO CHA MITIHANI.
Mitihani ya kitaifa kwa kidato cha nne KCSE, darasa la Nane KCPE na gredi ya sita KPSEA inapotarajiwa kuanza rasmi jumatatu wiki ijayo, kamishina wa kaunti ya Pokot magharibi Apolo Okelo amesema kwamba maandalizi yote yamekamilika kwa ajili ya mitihani hiyo.
Akizungumza na wanahabari afisini mwake, Apolo ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya usalama kaunti hiyo alisema kwamba kwa ushirikiano na idara ya elimu wameweka mikakati thabiti kuhakikisha kwamba mitihani hiyo inafanyika bila ya changamoto zozote za kiusalama wala usafiri.
“Tumejiandaa kikamilifu kwa ajili ya mitihani ya kitaifa. Hatutarajii changamoto yoyote wakati wa mitihani hiyo kwani tuna usalama wa kutosha, na pia tumefanya maandalizi ya magari ambayo yatatumika kusafirisha wasimamizi pamoja na makaratasi ya mitihani hadi vituo vya mitihani.” Alisema Apolo.
Apolo aliwataka walimu na watahiniwa wa maeneo ambayo yanakumbwa na utovu wa usalama kaunti hiyo kutokuwa na hofu kwani idara ya usalama imetuma maafisa wa kutosha katika kila kituo cha kufanyia mitihani, kuhakikisha kwamba watahiniwa wanafanyia mitihani yao katika mazingira salama.
“Kumekuwepo na hofu kwamba huenda kusifanyike mitihani katika baadhi ya shule kutokana na utovu wa usalama. Nawahakikishia wote kwamba hamna kituo hata kimoja ambacho kitakosa kuandaliwa mitihani, kwa sababu tumetuma maafisa wa usalama wa kutosha katika kila kituo cha mitihani.” Alisema.
Wakati uo huo Apolo alisema watashirikiana kikamilifu na wadau wote kuhakikisha mitihani hiyo inaendelea salama, akiwaonya vikali wasimamizi wa vituo vya mitihani dhidi ya kujaribu kufanikisha udanganyifu katika mitihani hiyo akisema watachukuliwa hatua.
“Tutakuwa na maafisa ambao watakuwa wakizunguka kuona jinsi mitihani hiyo inaendelea katika vituo mbali mbali vya mitihani. Na tunatoa onyo kwa wasimamizi wa vituo mbali mbali ambao watajaribu kufanikisha wizi wa mitihani kwamba watakaopatikana watachukuliwa hatua kali za kisheria.” Alisema.
Katika kaunti ya Pokot magharibi, kuna vituo 187 vya mitihani ya shule za upili KCSE, vituo 600 vya mitihani ya darasa la nane KCPE na vituo 683 vya mitihani ya gredi ya sita KPSEA.