WASIWASI WAKUMBA WAKULIMA TRANS NZOIA KUFUATIA KURIPOTIWA VIWAVI JESHI.


Wizara ya kilimo Kaunti ya Trans Nzoia imetangaza kuzuka kwa viwavi jeshi aina ya African fall army worm ambao wameripotiwa na wakulima maeneo mbalimbali Kaunti hiyo wakibainika kuwa hatari ikilinganishwa na walioripotiwa nchini miaka kadhaa iliyopita.
Kwenye mkao na wanahabari waziri wa Kilimo Kaunti ya Trans Nzoia Mary Nzomo amesema viwavi hao wana uwezo wa kuharibu asilimia kubwa ya mimea yoyote na wala sio mahindi pekee, akitoa wito kwa wakulima kutahadhari na kuripoti visa vyovyote vya uvamizi huo kwa wizara ya kilimo ili kupata usaidizi.
Wakati uo huo Waziri Nzomo amesema kama njia moja ya kuimarisha vita dhidi ya viwavi hao, Kaunti ya Trans Nzoia imepokea msaada lita 3,266 wa dawa ya kukabili wadudu hao waharibifu kutoka kwa serikali kuu akisema dawa hizo zitasambazwa kwa wakulima walioathirika bila malipo.
Nzomo ametoa wito wa msaada zaidi ikizingatiwa Kaunti ya Trans Nzoia ina zaidi ya ekari 105,000 ya mahindi na zaidi ya ekari 40,000 ya nyasi kwa mifugo ambayo ipo kwenye hatari ya kuvamiwa na viwavi hao.