WASHUKIWA WAWILI WA UVAMIZI WAUAWA NA POLISI CHESOGON.


Washukiwa wawili wa uvamizi wameuliwa kwa kupigwa risasi huku wengine wakiuguza majeraha mabaya kufuatia makabiliano makali na maafisa wa polisi usiku wa kuamkia leo eneo la chesogon mpakani pa kaunti hii ya Pokot magharibi na Elgeyo marakwet.
Joseph Lokanda chifu wa Kaben amesema kuwa wawili hao waliokuwa wakitumia pikipiki kuvuka mpakani waliuliwa na polisi baada ya polisi kushuku nia yao kuvuka mpakani usiku na ndipo wakawaagiza kusimama hali iliyopelekea kuzuka makabiliano ya risasi.
Aidha Okanda amesema kuwa uchunguzi umeanzishwa kubaini idadi kamili ya maafisa wa polisi waliojeruhiwa.
Miili ya wawili hao imepelekwa katika hospitali ya Tot huku waliojeruhiwa wakiendelea kupokea matibabu katika hospitali ya misheni ya Kapsowar.
Kisa hiki kinajiri wakati ambapo baadhi ya viongozi kutoka kaunti hii ya Pokot magharibi wameisuta serikali kufuatia utepetevu katika kuhakikisha uvamizi na wizi wa mifugo unakabiliwa eneo la bonde la kerio.