WASHUKIWA WA WIZI WA MIFUGO WAKANA KUHUSIKA WIZI.


Siku moja baada ya kushukiwa kupatikana na mali ya wizi eneo la marich kaunti hii ya Pokot magharibi na hata kufikishwa katika mahakama ya Kapenguria kabla ya kuachiliwa kwa bondi ya shilingi alfu 105, washukiwa hao wamekana vikali madai hayo yaliyotolewa na kamanda wa polisi eneo la Pokot ya kati.
Wakizungumza muda mfupi tu baada ya kuachiliwa kwa bondi na mahakama ya Kapenguria, wawili hao David njuguna na Edwin Muigai wamesema kuwa wao ni wafanyibiashara na walikuwa wametoka kununua mbuzi na kondoo waliodai kuiba katika soko la Takaywa.
Aidha Wawili hao wamekana madai ya kukaidi amri ya maafisa wa polisi kusimama katika kizuizi cha polisi cha marich ili kukaguliwa gari lao wakidai waliamua kuendelea na safari baada ya kusimama kwa muda bila kuhudumiwa na maafisa wa polisi waliokuwa katika kizuizi hicho, wakiwalaumu maafisa hao kwa kuwadhulumu wakati wa kisa hicho.
Jumanne wiki hii kamanda wa polisi eneo la Pokot ya kati Bamford surwa alidai kuwa wawili hao licha ya kuwa walikaidi amri ya polisi kusimama walidinda kueleza iwapo ni wamiliki halisi wa mifugo hao au la hali iliyopelekea polisi kushuku kuwa ni wezi wa mifugo.