WANASIASA WAONYWA DHIDI YA KUTUMIA MSAADA WA CHAKULA KUJIPIGIA DEBE.
Mwakilishi wadi maalum kaunti hii ya Pokot magharibi Elijah kasheusheu amepongeza hatua ya serikali kutoa msaada wa mahindi kwa ajili ya wakazi wanaokabiliwa na makali ya njaa maeneo mbali mbali ya kaunti hii.
Akizungumza na wanahabari Kasheusheu amesema kuwa mahindi haya yatafaa pakubwa familia zinazokabiliwa na makali ya njaa hasa wakati huu ambapo gharama ya maisha imezidi kupanda akiwataka wanasiasa kaunti hii kutotumia msaada huo kama chambo chao cha kutafuta kura.
Wakati uo huo Kasheusheu amewataka wakazi wa kaunti hii kutohadaiwa kuhusu yalikotoka mahindi hayo na kutoa wito kwa kamishina wa kaunti hii kufuatilia shughuli ya kugawa mahindi hayo ili kuhakikisha kwamba familia zinazokusudiwa zinafikiwa.
Serikali ya kitaifa inatarajiwa kutoa magunia alfu 100 kwa ajili ya familia zinazokabiliwa na makali ya njaa katika kaunti hii ya Pokot magharibi.