WANASIASA WALIOFELI KWENYE UCHAGUZI WAONYWA DHIDI YA KUHITILAFIANA NA UTENDAKAZI WA VIONGOZI WALIO MAMLAKANI.

Wito umetolewa kwa viongozi wa kisiasa katika kaunti ya Pokot magharibi hasa waliofeli katika uchaguzi mkuu uliopita kushirikiana na viongozi waliochaguliwa ili kuhakikisha kuwa wananchi katika kaunti hiyo wanapata huduma bora za maendeleo.

katibu wa kaunti hiyo Jonathan Siwanyang  alisema kwamba wakati wa siasa ulikamilika kwa uchaguzi wa mwezi agosti mwaka jana, na sasa ni wakati ambapo viongozi wote wanapasa kushirikiana na kuwahudumia wananchi.

Aliwataka wale walio na maoni tofauti na viongozi waliopo kwa sasa kusubiri hadi uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2027 ndipo waingie uwanjani kuwaomba wananchi kura.

“Ni wakati ambapo viongozi wa siasa waliofeli katika uchaguzi mkuu uliopita kukubali kwamba walishindwa na kushirikiana na viongozi waliochaguliwa katika kuwahudumia wananchi. Wakati wa siasa ulikamilika na iwapo kuna mtu aliye na maoni tofauti basi asubiri hadi uchaguzi mkuu ujao ndipo arudi uwanjani.” Alisema Siwanyang.

Wakati uo huo Siwanyang aliwapongeza wakazi wa kaunti hiyo kwa kuhakikisha kwamba wanakipa ushindi mkubwa chama cha UDA katika uchaguzi mkuu uliopita kwa kuhakikisha idadi kubwa ya viongozi waliochaguliwa ni wa chama hicho.

“Nashukuru kwamba wakazi wa kaunti hii walihakikisha kwamba wanawachagua viongozi wa chama cha UDA katika uchaguzi mkuu uliopita. Ingawa kwa sasa hali ni ngumu kidogo, lakini tunaomba tu muipe serikali muda kidogo, hali itakuwa sawa.” Alisema.