WANASIASA WALAUMIWA KUWA CHANZO CHA UTOVU WA USALAMA BONDE LA KERIO.
Viongozi wa kisiasa kutoka kaunti za bonde la kerio wamewahusisha baadhi ya wanasiasa na utovu wa usalama ambao umekithiri maeneo haya katika siku za hivi karibuni.
Wakizungumza katika hafla moja viongozi hao wakiongozwa na mbunge wa Kapenguria Samwel Moroto walitaka wanasiasa hao kukamatwa na kuchukuliwa hatua kali za kisheria badala ya kupoteza raslimali za serikali kwa kuendesha oparesheni za kiusalama maeneo haya.
“Nilisema hawa watu watatu wanajulikana kwa kuchochea watu. Wanasema maneno mengi ambayo yanapelekea utovu wa usalama. Hawa watu wanafaa kukamatwa na kuchukuliwa hatua badala ya kuharibu raslimaIi za serikali kwa kutuma maafisa wa polisi kuendesha oparesheni.” Alisema Moroto.
Ni kauli ambayo ilisisitizwa na mbunge wa Tiati William Kamket ambaye alitaka kuwepo na mikakati salama ya kuimarisha uhusiano baina ya jamii ambazo zinapatikana bonde la kerio badala ya kutekeleza oparesheni ambazo kulingana naye zinaegemea upande mmoja.
“Kunapasa kuwepo na mikakati ya kuimarisha uhusiano baina ya jamii zinazoishi katika eneo la bonde la kerio badala ya kila wakati kutuma maafisa wa usalama kufanya oparesheni ambazo zinawaumiza baadhi ya wakazi.” Alisema Kamket.