WANASIASA POKOT MAGHARIBI WATAKIWA KUTOHITILAFIANA NA MAJUKUMU YA WANAHABARI.
Seneta wa kaunti hii ya Pokot magharibi Samwel Poghisio amewasuta baadhi ya wanasiasa katika kaunti hii kwa kile amedai kutumia makundi ya vijana kuwatishia wanahabari wanapotekeleza majukumu yao ya kuwaarifu wananchi kinachojiri katika kaunti hii.
Akizungumza na kituo hiki Poghisio amedai kutishiwa baadhi ya wanahabari ambao walikuwa wakifuatilia shughuli ya ugavi wa chakula cha msaada ambacho kilitolewa na serikali kuu kwa ajili ya wakazi wa kaunti hii wanaokabiliwa na makali ya njaa.
Poghisio amesema wanahabari hao walikuwa wakitekeleza shughuli zao kulingana na taaluma yao na si haki kwa kiongozi yeyote wa kisiasa kutumia makundi ya wahuni kuhujumu utendakazi wao kwa kuwatishia.
Amedai baadhi ya wanasiasa katika kaunti hii walitaka kutumia chakula hicho kutafuta uungwaji mkono kutoka kwa wananchi wakidai kimetolewa nao kabla ya njama hiyo kutibuliwa na wanahabari.
Poghisio amewataka wanahabari katika kaunti hii kutotishwa na visa kama hivyo na badala yake kutekeleza majukumu yao ya kutoa habari hasa kuhusu maswala yanayohusu mwananchi kwani wamehakikishiwa usalama wao.