WANAOPINGA MIPANGO YA KUAGIZWA MAHINDI KUTOKA MATAIFA YA NJE WASUTWA VIKALI.

Mjadala kuhusu uagizaji wa mahindi kutoka nje ya nchi ukiendelea kushika kasi nchini, baadhi ya wakazi wa kaunti ya Pokot magharibi wameunga mkono swala hilo wakiwataka wanaopinga kukoma kuingiza siasa katika swala hilo.

Wakazi hao walisema kwamba kwa sasa hamna mahindi ya kutosha humu nchini ya kukidhi mahitaji ya wakenya kwani wakulima wengi hawakupanda viwango vya kutosha vya mahindi kutokana na gharama ya juu ya pembejeo.

Walisema kwamba kwa sasa wakenya wengi wanakabiliwa na makali ya njaa na ipo haja ya serikali kuchukua hatua za dharura kuwaokoa wakenya kutokana na hali hiyo kwa kuagiza mahindi ya kutosha kutoka mataifa ya nje.

Nawaeleza wabunge katika taifa hili waachane na serikali iagize chakula ili kuwepo na chakula cha kutosha katika taifa hili. Wakenya wengi kwa sasa wanakabiliwa na makali ya njaa na ilivyo sasa hamna mahindi ya kutosha kutosheleza mahitaji ya wakenya ikizingatiwa bei ghali ya pembejeo haikuwaruhusu wakulima kupanda viwango vya juu vya mahindi.” Walisema 

Aidha wakazi hao walidai kwamba wabunge na viongoz mbali mbali wanaopinga uagizaji wa mahindi hayo hawafanyi hivyo kwa maslahi ya wakenya bali ni kwa manufaa yao wenyewe kwa kushirikiana na wafanyibiashara wanaowapunja wakenya.

“Wengi wa wabunge ambao wanapinga hatua ya serikali kuagiza mahindi kutoka nje wanafanya hivyo kwa maslahi yao wenyewe. Wabunge hao wanafanya hivyo kwa sababu sasa wamenunua mahindi kutoka kwa wakulima na sasa wanasubiri bei ipande ndio wawanyanyase wakenya kwa kuwauzia kwa bei ghali.” Walisema.