WANAOENDESHA OPARESHENI YA KIUSALAMA BONDE LA KERIO WATAKIWA KUDUMISHA NIDHAMU KATIKA SHUGHULI NZIMA.

Viongozi katika kaunti ya Pokot magharibi wameendelea kutoa wito kwa maafisa wa usalama ambao wanaendesha oparesheni ya kiusalama katika kaunti 6 za kaskazini mwa bonde la ufa kuiendesha kwa utaratibu ili kuzuia mahangaiko miongoni mwa wakazi wa maeneo hayo wasio na hatia.

Wa hivi punde kutoa wito huo ni aliyekuwa mwaniaji kiti cha ubunge eneo la bunge la Pokot kusini James Teko ambaye alisema kwa sasa wananchi wanapitia hali ngumu ya maisha ikiwemo uhaba wa maji na chakula na hawafai kuongezewa mahangaiko mengine kufuatia oparesheni hiyo.

Tunaomba maafisa wa usalama ambao wanaendesha oparesheni ya kiusalama katika kaunti za kaskazini mwa bonde la ufa, kuwafanya kazi hiyo kwa nidhamu na kuhakikisha kwamba wanakabiliana na hao majangili pekee ili wananchi ambao hawana hatia waendelee na maisha yao bila mahangaiko.” Alisema Teko.

Aidha Teko alisema kwamba kando na kutumia nguvu kutwaa silaha zinazomilikiwa kinyume cha sheria miongoni mwa wakazi, mazungumzo ya amani yanafaa kupewa kipau mbele kwani chimbuko kuu la utovu wa usalama maeneo haya ni mizozo kuhusu raslimali kama vile malisho ya mifugo na maji.

“Wakati mwingine inafaa kuangalia vizuri kufahamu ni nini kinafanyika. Kwa sababu tatizo kuu la maeneo haya ni ukosefu wa malisho kwa mifugo pamoja na maji. Matumizi ya nguvu, ndio yatasaidia kupunguza baadhi ya mizozo lakini kwa amani ya kudumu inafaa kuwa na mazungumzo ya amani katika pande zote husika.” Alisema.

Wakati uo huo Teko alitoa wito kwa viongozi kutoka pande zote zinazozozana kujitenga na matamshi ambayo huenda yakachochea uhasama miongoni mwa wakazi akisema mkenya yeyote ana haki ya kuishi sehemu yoyote ya taifa hili.

“Ninachoomba watu wetu ni kwamba tusichochee hali hii kwa kutaka baadhi ya watu kuhama maeneo fulani kwa sababu ni haki ya kila mkenya kuishi mahali popote hapa nchini bila kushurutishwa kuondoka.” Alisema.