WANANCHI WATAKIWA KUTAHADHARI MVUA YA ELNINO INAPOTARAJIWA.
Wakazi wa kaunti ya Pokot magharibi hasa wanaoishi maeneo ambayo yana historia ya maporomoko ya ardhi wametakiwa kutahadhari pakubwa wakati huu ambapo mvua ya Elnino inatarajiwa kulingana na utabiri wa hali ya anga.
Ni wito wake waziri wa barabara na uchukuzi kaunti hiyo Joshua Ruto ambaye hata hivyo aliwataka wakazi kutumia msimu huu wa mvua katika kuendeleza kilimo cha mimea ili kuwe na chakula cha kutosha na kukabili makali ya njaa ambayo hushuhudiwa msimu wa kiangazi.
Aidha Ruto aliwahimiza wakazi kutovuka kiholela mito inayofurika kunaponyesha mvua ili kuzuia maafa ambayo huenda yakatokea.
“Mvua huja na hasara na pia na faida zake. Kwa hivyo mimi nawahimiza wakazi wa kaunti hii hasa wanaoishi maeneo yenye historia ya maporomoko ya ardhi kutahadhari. Pia tusiangazie tu madhara ambayo huenda yakatokana na mvua hiyo bali pia tuhakikishe kwamba tunaitumia kuendeleza kilimo kwa kupanda vyakula ambavyo vitatusaidia wakati wa ukame.” Alisema Ruto.
Wakati uo huo waziri Ruto aliwahakikishia wakazi wa maeneo mbali mbali ya kaunti hiyo kwamba serikali ya kaunti inaendelea kushughulikia changamoto za barabara ili kuhakikisha kwamba shughuli za uchukuzi zinarahisishwa.“Serikali kupitia idara ya barabara inaendelea kushughulikia barabara mbali mbali ili kuhakikisha kwamba shughuli za uchukuzi hazitatiziki kutokana na ubovu wa barabata na pia kuwawezesha wakulima wetu kifikisha mazao yao sokoni kwa wakati.” Alisema