WANANCHI WATAKIWA KUMPA MUDA RAIS RUTO ANAPOENDELEA KUSHUGHULIKIA GHARAMA YA MAISHA.

Baadhi ya viongozi katika kaunti ya Pokot magharibi wamemtetea rais William Ruto kutokana na shutuma ambazo zinaelekezwa kwa serikali yake kufuatia sera mbovu za kufufua uchumi ambazo zimetajwa kupelekea kupanda kwa gharama ya maisha.

Wakiongozwa na mbunge wa Sigor Peter Lochakapong, viongozi hao waliwataka wakenya kuwa watulivu na kumpa muda rais Ruto anapoendelea kuweka mikakati ya kuhakikisha kwamba gharama ya maisha inateremka.

Lochakapong alisema kwamba hatua ya rais Ruto kuteremsha bei ya mbolea pamoja na kuwekeza zaidi katika mitambo ya kukausha mahindi ni baadhi tu ya mikakati inayoashiria kujitolea kwa serikali yake kuhakikisha hali ngumu ambayo inawakabili wananchi inashughulikiwa.

“Tunajua kwamba gharama ya maisha imepanda sana nchini, lakini kile tunaomba wananchi ni kwamba wawe na subira na kumpa rais muda katika mikakati ambayo anaendeleza kuhakikisha hali inarejea kawaida. Tayari kuna mikakati ambayo ameweka ikiwemo kupunguza bei ya mbolea kwa sababu tunafahamu fika kwamba gharama ya maisha mara nyingi huzungukia chakula.” Alisema Lochakapong.

Wakati uo Lochakapong aliwasuta wanaoendeleza ukosoaji kwa serikali ya rais Ruto akisema kwamba hawaangazii mazuri ambayo tayari ametekeleza hadi kufikia sasa mwaka mmoja tangu aingie mamlakani, ikiwemo kuajiri idadi kubwa zaidi ya walimu ikilinganishwa na serikali zilizotangulia.

“Wale ambao wameendelea kushutumu uongozi wa rais Ruto hawaangazii mema ambayo ametekeleza hadi kufikia sasa tangu alipoingia uongozini. Kwa mfano katika historia ya taifa hili ni rais Ruto pekee ambaye ameweza kuajiri walimu wengi kwa wakati mmoja ikilinganishwa na serikali zilizotangulia.” Alisema.