WANANCHI WATAKIWA KUIPA MUDA SERIKALI INAPOFANYIA MAGEUZI IDARA YA AFYA.

Katibu katika wizara ya afya Mary Muthoni ametoa wito kwa wakazi katika kaunti ya Pokot magharibi kuipa muda idara ya afya kutokana na mageuzi ambayo yanafanyika kwenye idara hiyo hasa kufuatia hatua ya idara hiyo kuwaajiri wahudumu wa afya wa nyanjani kuwafikia wananchi walio maeneo ya mashinani.

Akizungumza mjini Kapenguria, Muthoni alisema kwamba idara hiyo ingali inapitia mageuzi na serikali ipo tayari kurekebisha mianya yoyote ambayo itatokea katika mageuzi hayo ili kuhakikisha kwamba wananchi wanapata huduma za afya kwa viwango vinavyostahili.

Muthoni alisema kwamba kuajiriwa kwa maafisa hao wa nyanjani kutasaidia serikali kufahamu changamoto hasa za kijiografia ambazo zinawakumba wakazi wa maeneo husika katika kuafikia huduma za afya na kuchukua hatua ili kusuluhisha changamoto hizo.

“Serikali inafanya kazi kulingana na mipangilio yake. Na kwa sababu ndio mwanzo tumeanza mageuzi haya, ni muhimu kuipa serikali muda ili tuone mianya iliyopo ndipo tuweze kuishughulikia.” Alisema Muthoni.

Wakati uo huo Muthoni alisema kwamba maafisa wa wizara ya afya wamezuru zaidi ya vituo alfu 15 maeneo mbali mbali ya nchi, na wana rekodi za mahitaji yote ya vituo hivyo, akisema kwamba idara hiyo inaendeleza mikakati ya kuhakikisha kwamba mahitaji hayo yanashughulikiwa.

“Kama wizara tumezuru takriban vituo alfu 15 kote nchini na tunafahamu changamoto ambazo kila kituo kinapitia. Kwa sasa tunaweka mikakati ya kuhakikisha kwamba changamoto hizo zinashughulikiwa.” Alisema.

[wp_radio_player]