WANANCHI WA LOKICHAR NA MASOL WANUFAIKA NA CHAKULA KUTOKA KWA BENKI YA KCB KAUNTI YA POKOT MAGHARIBI

Benki ya KCB tawi la Pokot magharibi kupitia wakfu wa KCB foundation imezindua mpango wa siku mbili wa kutoa chakula cha msaada kwa wakazi wa lokesheni za Lokichar eneo la Kacheliba na Masol eneo bunge la Sigor.

Akizungumza wakati wa zoezi hilo lililogharimu kima cha shilingi milioni moja, meneja wa benki hiyo Paul Mutai amesema kwamba wamelenga familia 150 zilizotambuliwa katika kila lokesheni hizo ambazo zimeathirika zaidi na na baa la njaa.

Mutai amesema kwamba benki hiyo ilitambua lokesheni hizo mbili kwa ushirikliano na mamlaka ya kukabili majanga NDMA kutokana na hali kuwa wakazi wa maeneo hayo hawajafikiwa na misaada ambayo imekuwa ikitolewa na wahisani wengine.

Akipongeza benki ya KCB kwa msaada huo, afisa katika mamlaka ya NDMA Joshua Mayeku amesema kwamba familia nyingi katika kaunti hii zinakabiliwa na baa la njaa kutokana na ukame wa muda mrefu uliosababisha wakazi wengi kutopata mavuno mwaka huu akiwataka wahisani zaidi kujitokeza.

Wakazi wa eneo hilo walionufaika na msaada huo wameipongeza benki ya KCB japo wakiitaka kuongeza kiwango cha msaada huo ili kuwafikia wakazi zaidi.