WANANCHI POKOT MAGHARIBI WATAKIWA KUJITOKEZA KUSHIRIKI ZOEZI LA KITAIFA LA UPANZI WA MITI.

Kaunti ya Pokot magharibi inaungana na maeneo mengine nchini kuendeleza shughuli ya kitaifa ya upanzi wa miti hii leo ikizingatiwa ilitangazwa kuwa siku ya kitaifa ya mapumziko ili kutoa nafasi kwa wananchi wote kushiriki zoezi hilo.

Shughuli hiyo inaongozwa na waziri wa afya Suzan Nakhumicha katika kaunti hiyo ambaye ataongoza shughuli hiyo pia katika kaunti jirani ya Elgeyo marakwet.

Akizungumza jumapili alipozuru kaunti ya Pokot magharibi kabla ya kutekelezwa shughuli hii rasmi hii leo, Waziri Nakhumicha alisema kwamba analenga kuhakikisha miti milioni 5 inapandwa kila mwaka katika kaunti hizo mbili ili kuafikia lengo la miti milioni 50 kwa kipindi cha miaka kumi.

“Mimi nimepewa na rais kaunti mbili ikiwemo kaunti hii ya Pokot magharibi na kaunti ya Elgeyo Marakwet kusimamia upanzi wa miti. Na nimepewa lengo la miti milioni 50 kwa miaka kumi. Kwa hivyo katika miaka kumi ambayo nimepewa kusimamia shughuli hii, ninalenga kuhakikisha miti milioni 5 inapandwa kila mwaka katika kaunti hizi mbili.” Alisema Nakhumicha.

Gavana wa kaunti hiyo Simon Kachapin alisema kwamba serikali yake itashirikiana kikamilifu na waziri pamoja na maafisa wake kuhakikisha kwamba idadi inayohitajika ya miti inapandwa kaunti hiyo ikizingatiwa ni moja ya kaunti ambazo zinaathirika pakubwa na mabadiliko ya hali ya anga.

“Mimi ninaahidi kujitolea kushirikiana na wazir kuhakikisha kwamba tunapanda miti ambayo rais ameagiza, ikizingatiwa kwamba kaunti hii imeathirika kutokana na mabadiliko ya hali ya anga.” Alisema Kachapin.