WANAHARAKATI NORTH RIFT WATAJA AGIZO LA WIZARA YA USALAMA KUWA NJAMA YA UNYAKUZI WA ARDHI.

Hisia mseto zimeendelea kuibuliwa kufuatia agizo la waziri wa maswala ya ndani ya nchi Prof. Kithure Kindiki la kuwataka wakazi wa maeneo yaliyooredheshwa kuwa maficho ya wezi wa mifugo katika kaunti sita za kaskazini mwa bonde la ufa kuondoka ili kupisha awamu ya pili ya oparesheni ya kuwakabili wahalifu hao.

Wa hivi punde kuzungumzia swala hilo ni mwanaharakati wa haki za binadam kaunti ya Pokot magharibi Abraham Kibet ambaye amesuta vikali agizo hilo la waziri Kindiki akidai kwamba ni njama ya watu wenye ushawishi serikalini kunyakua ardhi maeneo hayo.

Kibet alisema kwamba kwa sasa wakenya wengi hasa kutoka jamii za wafugaji tayari wanakabiliwa na hali ngumu ya maisha kufuatia ukame ambao umeshuhudiwa maeneo haya, na ni kuwahangaisha kwa kuwaongezea tena mzigo wa kuwa wakimbizi.

“Mambo yanayoendelea sasa hayahusiani na usalama. Hilo agizo ambalo lilitolewa na waziri wa usalama kuwataka wakazi wa maeneo haya kuondoka sasa linaonyesha kwamba huu ni mpango wa watu wenye ushawishi serikalini kunyakua ardhi za wakazi wa meneo hayo.” Alisema Kibet.

Kibet sasa anatoa wito kwa serikali kubatilisha mara moja agizo hilo na badala yake kutumia mbinu tofauti kuwakabili wahalifu hao bila kusababisha mahangaiko kwa wakazi wa maeneo husika.

“Serikali inapasa kusitisha mara moja agizo hilo. Kama ni swala la usalama, wangetafuta wahalifu na kukabiliana nao. Watafute wazee wa mitaa, machifu na wakuu wa makanisa ili wasaidie katika kuwatambua watu wachache ambao wanasababisha utovu wa usalama ila si kuwahangaisha wananchi kwa kuwahamisha maeneo yao.” Alisema.