WANAHARAKATI BUNGOMA WATAKA USHIRIKIANO NA SERIKALI YA KAUNTI


Wanaharakati katika kaunti ya Bungoma wameitaka serikali ya kaunti hiyo kushirikiana na mashirika ya kijamii ili kuimarisha mazingira ya utendakazi na kuboresha huduma kwa umma.
Wakiongozwa na Lumumba Wekesa wanaharakati hao wamesema kuwa mashirika ya kijamii katika kaunti hiyo yamepuuzwa na serikali ya kaunti hiyo kwani michango yao katika kuhakikisha huduma bora kwa wakazi haidhaminiwi.
Wakati uo huo wanaharakati hao wametaka mivutano ambayo inashuhudiwa kati ya bunge la kaunti hiyo ya Bungoma na gavana Wyclife Wangamati kutafutiwa suluhu haraka ili kuepuka hali ya kulemazwa huduma kwa umma.
Wanaharakati hao walikuwa wakizungumza baada ya kongamano lao la kila mwaka ambapo wamesema kongamano la mwaka huu linalenga kutoa uhamasisho zaidi kuhusu majukumu ya wanaharakati katika ushirikiano baina yao na serikali ya kaunti.