WANAFUNZI WAFAIDI NA MPANGO WA KCB FOUNDATION POKOT MAGHARIBI
Benki ya KCB kupitia wakfu wa KCB foundation inaendelea kuweka mikakati ya kuwafadhili wanafunzi zaidi werevu kutoka jamii zisizojiweza kaunti hii ya Pokot magharibi.
Akizungumza baada ya kukutana na wanafunzi ambao wanafadhiliwa na wakfu huo, meneja wa benki hiyo tawi la Pokot Magharibi Paul Mutai amesema kwamba benki hiyo itaendelea kuwafadhili wanafunzi hao hadi vyuo vikuu kwa wale watakaofanikiwa kujiunga na vyuo hivyo.
Mutai ametumia fursa hiyo kuwataka wazazi na jamii kwa jumla kuwatunza vyema wanao msimu huu wa sherehe nyingi na kuwaepusha na tamaduni zilizopitwa na wakati kama vile ukeketaji na ndoa za mapema ili kuhakikisha kwamba wanarejea shuleni wakiwa katika hali nzuri shule zitakapofunguliwa baadaye mwezi januari.
Baadhi ya wanafunzi wanaofadhiliwa na benki hiyo wameelezea shukurani zao kwa benki hiyo kwa kuwafadhili, mmoja wa washauri katika wakfu wa KCB Edwin Chumba akiwataka wazazi na walezi kutilia mkazo swala la elimu kwa wanao kwa manufaa yao ya baadaye.