WANAFUNZI ELFU 1,070 WALIPACHIKWA MIMBA WAKATI WA LIKIZO YA CORONA KAUNTI YA POKOT MAGHARIBI


Jumla ya wanafunzi 1,070 walipachikwa mimba katika kaunti hii ya Pokot Magharibi wakati wakiwa nyumbani katika likizo ndefu iliyotokana na kufungwa shule baada ya kuripotiwa maambukizi ya virusi vya corona nchini.
Akitoa takwimu hizi katika mkutano ulioandaliwa na shirika la kushughulikia maswala ya watoto duniani AMREF, John Simiyu aliyemwakilisha mkurugenzi wa elimu kaunti hii Jacob Onyiego, amesema wanafunzi 662 ni wa shule za upili huku 408 wakiwa kutoka shule za msingi.
Simiyu amewashauri walimu kuwafunza wanafunzi kuhusu mbinu za maisha yani “life skills” pamoja na kuzingatia zaidi ushauri nasaha ili kukabili hali hii.
Mshirikishi wa baraza la waislamu SUPKEM kanda ya bonde la ufa Haji Omar Jumbe aliyehudhuria mkutano huo amewalaumu pakubwa wazazi kwa kuchangia kukithiri visa hivi kwa kuwatelekeza wanao.
Ni kauli ambayo imetiliwa mkazo na mwakilishi wadi maalum Elijah Kasheusheu ambaye amewataka wadau kushirikiana katika kupiga jeki juhudi za kukabili mimba za mapema miongoni mwa wanafunzi.
Mwanachama wa kamati ya sauti sasa iliyobuniwa na Shirika la AMREF itakayojukumika kuendeleza hamasisho kwa jamii kuhusu athari za mimba za mapema kaunti hii Loise Cherop, ametoa wito kwa jamii pamoja na viongozi wa mitaa kushirikiana nao ili kufanikisha juhudi hizi.