WANAFUNZI ALFU MOJA WA KIKE POKOT KASKAZINI WANUFAIKA NA SODO KUPITIA MPANGO WA BEYOND ZERO.
Idara ya afya kaunti ya Pokot magharibi imepokea sodo alfu moja kutoka kwa mpango wa beyond zero, ambao unatarajiwa kuendelea kusambaza vitambaa hivyo kila muhula kwa kipindi cha mwaka mmoja ujao katika shule 10 za msingi pokot kaskazini.
Akizungumza wakati akipokea vifaa hivyo afisa wa kitengo cha afya ya akina mama na watoto kwenye wizara ya afya kaunti hiyo Consolata Sire alisema sodo hizo zitasambazwa katika shule za msingi 10 hasa eneo la pokot kaskazini.
Sire alipongeza mpango huo anaosema kwamba ni muhimu zaidi katika kuhakikisha kwamba wanafunzi hawakosi kuhudhuria masomo kwa kukosa vitambaa hivyo katika siku zao za hedhi.
“Siku ya leo tumepokea sodo alfu moja kutoka kwa mpango wa beyond zero, na tunatarajia kuzisambaza katika shule 10 eneo la pokot kaskazini. Hawa watoto wamekuwa wakipata changamoto sana wakati wa siku zao za hedhi lakini sasa wataendelea vyema na masomo yao kwani hawatakuwa na la kuhofia.” Alisema Sire.
Msimamizi wa wauguzi katika kaunti hiyo Dinah Poghisio alisema kwamba hatua hiyo itawafanya watoto wa kike kuwa na ujasiri wa kukaa na wenzao wa kiume kutokana na hali kwamba sasa hawatalazimika kupitia unyanyapaa wakati wa siku zao za hedhi.
“Hamna kitu ambacho sasa kinaweza kuwazuia watoto wa kike kusoma kwa kuwa watapata nafasi ya kukaa na wenzao hasa wa kiume bila ya kuwa na wasiwasi wa kupitia unyanyapaa wakati wa hedhi.” Alisema Poghisio.