WANAFUNZI 496 WAREJESHWA SHULENI KUFUATIA OPARESHENI ILIYOENDESHWA KACHELIBA.


Zaidi ya wanafunzi 400 katika kaunti ndogo ya kacheliba kaunti hii ya Pokot magharibi waliweza kurejeshwa shuleni katika oparesheni iliyoendeshwa eneo hilo na wadau wa elimu kwa ushirikiano na shirika la kushughulikia watoto UNICEF.
Haya ni kwa mujibu wa mkurugenzi wa elimu eneo la Kacheliba Edward Wangamati ambaye amesema kuwa kati ya wanafunzi 496 waliorejeshwa shuleni eneo hilo, 250 walikuwa wavulana huku wanafunzi wa kike wakiwa 246.
Wangamati amesema japo shughuli hiyo ilipokelewa vyema na baadhi ya wazazi, walikabiliwa na changamoto katika kuwashawishi baadhi yao kwani wapo waliowaficha watoto wao na hata wengine kulazimika kutorokea taifa jirani la Uganda.
Amesema kuwa mtindo wa maisha kwa wakazi wengi wa kaunti hii ya Pokot magharibi ndicho kizingiti kikuu kwa elimu ya watoto wengi kwani wazazi wengi wanathamini zaidi mifugo kuliko elimu ambapo watoto wengi wanalazimika kusalia nyumbani ili kulisha mifugo.