WAMILIKI WA SILAHA HARAMU KAUNTI YA POKOT MAGHARIBI WAPEWA MAKATAA YA SIKU SABA KUZISALIMISHA.
Zaidi ya bunduki 60 zimerejeshwa katika oparesheni ya kiusalama ambayo inaendelezwa na maafisa wa usalama maeneo ya mipakani pa kaunti ya Pokot magharibi na kaunti jirani ikiwemo Turkana, Elgeyo Marakwet na Baringo.
Akizungumza katika mkutano wa amani ambao uliwaleta pamoja wakazi wa eneo la Turkwel na maafisa wa usalama, kamanda wa polisi katika kaunti hiyo Peter Katam aidha alisema kwamba zaidi ya risasi alfu moja zimepatikana, huku akitoa makataa ya wiki moja kwa wakazi ambao bado wanamiliki silaha hizo kuzirejesha.
“Kufikia sasa tumepata bunduki 62 kufuatia oparesheni ya kiusalama ambayo inaendeshwa eneo hili, na risasi zaidi ya alfu moja. Ninachowahimiza wananchji ni kwamba wale ambao bado wanamiliki silaha hizo wana wiki moja kuzisalimisha la sivyo tutamia nguvu kuzitwaa.” Alisema Katam.
Naibu kamishina wa eneo bunge la Kapenguria Wyclife Munanda alishutumu machafuko ambayo yalishuhudiwa siku chache zilizopita na kuathiri shule moja eneo hilo aliyotaja kuwa yalisababishwa na propaganda za kikabila huku akiwahakikishia wakazi kwamba usalama umeimarishwa.
“Kulikuwa na propaganda za kikabila ambazo zilienezwa eneo hili na watu ambao hawataki amani na kupelekea machafuko ambayo yalishuhudiwa siku chache zilizopita. Lakini kwa sasa tunawahakikishia wananchi kwamba serikali itahakikisha amani inadumu eneo hili.” Alisema Munanda.
Wakazi eneo hilo wakiongozwa na chifu wa kositei Siroyo Afrikana walitoa wito kwa serikali kuhakikisha kwamba shule zinalindwa na maafisa wa NPR ili kuwahakikishia usalama wanafunzi hasa wakati huu ambapo mitihani ya kitaifa inakaribia.
“Tunaomba kwamba serikali iwaajiri maafisa wa NPR ambao watahakikisha shule zinakuwa salama hasa wakati huu ambapo wanafunzi wa darasa la nane na kidato cha nne wanatarajiwa kufanya mitihani yao ya kitaifa.” Walisema wakazi.