WALIOHAMA KUTOKANA NA UTOVU WA USALAMA MIPAKANI PA KAUNTI YA POKOT MAGHARIBI WAHIMIZWA KUREJEA.
Mwakilishi wadi ya Siyoi kaunti ya Pokot magharibi Esther Serem ametoa wito kwa wakazi waliohama makwao kutokana na utovu wa usalama hasa maeneo ya mipakani pa kaunti ya Pokot magharibi, kurejea kufuatia mikakati ambayo serikali imeweka kuhakikisha usalama maeneo hayo.
Serem alisema hatua ya serikali kuajiri maafisa wa akiba NPR itasaidia pakubwa kuhakikisha kwamba usalama unadumishwa, na pia kufanikisha juhudi za kuhakikisha shughuli za masomo ambazo zilisambaratishwa eneo hilo na wahalifu zinarejelewa.
Aidha Serem aliwahimiza wakazi wa maeneo hayo kudumisha amani na majirani zao ili kuhakikisha kwamba wanafunzi wanapata mazingira bora ya kuendeleza masomo yao hasa baada ya kuathirika kwa muda mrefu.
“Nawahimiza wakazi ambao walihama makwao kutokana na ukosefu wa usalama mikapani pa kaunti hii kurudi nyumbani, kwa sababu sasa serikali imeweka mikakati ya kutosha kuhakikisha kwamba kuna amani ya kutosha, na ambayo itawasaidia wanafunzi kurejelea masomo.” Alisema Serem.
Aidha Serem ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya elimu katika bunge la kaunti ya Pokot magharibi alitoa wito kwa walimu ambao watatumwa kufunza katika shule hizo kuwakaribia zaidi wanafunzi hao na kuwashauri kila mara kwani wameathirika pakubwa na hali ya utovu wa usalama.
“Nawahimiza walimu ambao watatumwa maeneo hayo kwamba wawe karibu na wanafunzi na kuwatia moyo, kwa sababu tunaelewa kwamba huenda wameathiriwa pakubwa kutokana na maswala haya ya utovu wa usalama, ambao wamekumbana nao kwa miaka mingi.” Alisema.