WALIMU WAONYWA DHIDI YA KUWASAJILI WANAFUNZI WA GREDI YA SITA KUFANYA MTIHANI WA DARASA LA NANE KCPE.
Idara ya elimu eneo la Pokot kusini katika kaunti ya Pokot magharibi imewaonya vikali wazazi na walimu wakuu wa shule mbali mbali dhidi ya kuwasajili wanafunzi waliofanya mtihani wa gredi ya sita kuwa watahiniwa wa mtihani wa darasa la nane KCPE.
Akizungumza wakati wa ufunguzi rasmi wa chumba cha mankuli katika shule ya msingi ya Kamelei, mkurugenzi wa elimu eneo la Pokot kusini Charles Kitur alisema kwamba wana habari kuhusiana na visa hivyo akitoa wito kwa idara za usalama kufanya uchunguzi na kuhakikisha wanaoendeleza shughuli hiyo wanakabiliwa kisheria.
“Tuna habari kwamba kuna baadhi ya wakuu wa shule eneo hili ambao wanashirikiana na wazazi kuwasajili wanafunzi waliofanya mtihani wa gredi ya sita kufanya mtihani wa darasa la nane KCPE. Haya ni makosa makubwa na watakaopatikana wanafanya hivyo watachukuliwa hatua za kisheria.” Alisema Kitur.
Aidha Kitur alitumia fursa hiyo kutoa wito kwa wazazi eneo hilo na kaunti ya Pokot magharibi kwa ujumla kukumbatia elimu kwa wanao akisema kwamba ni kupitia tu elimu ambapo kutashuhudiwa amani kaunti hii kando na kuhakikisha maisha bora katika siku zao za usoni.
“Nawahimiza wazazi kufahamu umuhimu wa elimu kwa wanao. Ni kupitia elimu tu ambapo tutakuwa na usalama eneo hili. Ni kupitia kwa watoto wetu kusoma ndipo tutapunguza visa vya matumizi ya dawa za kulevya miongoni mwa vijana. Pia ni elimu hiyo ndiyo itaimarisha maisha yetu na ya watoto wetu.” Alisema.
Ni kauli ambayo ilisisitizwa na mwalimu mkuu wa shule hiyo Solomon Kiplagat ambaye aidha alisema kwamba tayari tume ya huduma kwa walimu TSC imetuma walimu wawili katika shule hiyo kuwahudumia wanafunzi wa gredi ya saba, akikariri pia uwepo wa vitabu kwa ajili ya wanafunzi hao.
“Natoa wito kwa wazazi walete watoto wao shuleni. Kwa sasa tunashukuru tume ya TSC kwa kututumia walimu wawili wa gredi ya saba na pia kuna vitabu vya kutosha ambavyo watoto hao watatumia.” Alisema Kiplagat.