WALIMU WAKUU WAONYWA DHIDI YA KUWATUMA NYUMBANI WANAFUNZI KUTAFUTA KARO.

Chama cha walimu wa shule za upili na vyuo vya kadri KUPPET tawi la Pokot magharibi kimetoa wito kwa walimu wakuu kutowatuma nyumbani wanafunzi kutafuta karo.

Akizungumza afisini mwake katibu mkuu wa chama hicho Alfred Kamuto aliwataka wakuu hao kuwa na subira wakati gavana Simon Kachpin akiendeleza mikakati ya kuhakikisha kwamba fedha za basari zinatumwa shuleni kufadhili masomo ya wanafunzi.

Kamuto amesema haitakuwa bora kwa wakuu wa shule kuwatuma nyumbani wanafunzi wakati serikali ya kaunti kupitia gavana Kachapin imetoa hakikisho la kutoa fedha hizo hivi karibuni baada ya kukamilika zoezi la kukagua orodha ya wanafunzi waliotuma maombi ya ufadhili huo.

“Nawahimiza wakuu wa shule zote za kaunti hii kuwa na subira na kutowatuma nyumbani wanafunzi wakati gavana wa akiendeleza mikakati ya kuhakikisha kwamba shule zinapata fedha za basari. Nina uhakika kwamba hayatapita majuma mawili kabla ya kukamilika zoezi la kukagua orodha ya waliotuma maombi.” Alisema Kamuto.

Wakati uo huo Kamuto alitoa wito kwa machifu kwa ushirikiano na wazee wa mitaa pamoja na walimu kuhakikisha kwamba watoto ambao hawajaenda shuleni hadi kufikia sasa wanafanya hivyo kuambatana na sera ya serikali ya kuhakikisha kwamba wanafunzi wote wanakwenda shule.

“Nawahimiza pia machifu kwa ushirikiano na wazee wa mitaa kuhakikisha kwamba watoto wote ambao wangali nyumbani wanaenda shule. Kwa sababu serikali inalenga kuhakikisha kila mwanafunzi anahudhuria masomo chini ya sera ya mpito wa asilimia mia moja.” Alisema.