WALIMU WAKUU KAUNTI YA POKOT MAGHARIBI WAPUUZILIA MBALI AGIZO LA WIZARA YA ELIMU


Walimu wakuu kaunti ya Pokot Magharibi wamepuuzilia mbali agizo la waziri wa elimu Proff George Magoha la kutowatuma nyumbani wanafunzi kutokana na karo.
Wiki hii kaunti ya Pokot Magharibi wanafunzi wengi wa shule tofauti tofauti wameonekana mjini makutano wakirandaranda huku wakihoji kwamba wametumwa nyumbani karo ya shule .
Kulingana na wazazi waliozungumza na Kalya Radio mapema leo mjini Makutano wamehoji kwamba kuna changamoto chungu nzima katika baadhi ya shule mjini Makutano ikiwemo ukosefu wa maji na chakula wazazi wakidai kwamba kuna baadhi ya karo ambayo walilipa mwanzoni mwa mwaka jana na kuwataka walimu wakuu kuitumia badala ya wanafunzi kuonekana barabarani mara kwa mara.
Hata hivyo baadhi ya wazazi kaunti hii wamesema kwamba waliwatuma wanafunzi shuleni na kiasi kidogo cha karo na sasa chakushangaza ni kwamba wanafunzi waliolipa kiasi hicho kidogo na hata waliokosa kulipa wote wanatumwa jambo ambalo ni la kusikitisha kwa mzazi ambaye anajikakamua kila siku.
Kadhalika wazazi wengine wanasema wanapitia changamoto chungu nzima kwa biashara zao ikizingatiwa kwamba ni Januari.
Ikumbukwe mapema mwezi huu waziri Magoha alisema kuwa kima cha shilingi bilioni nne tayari zimetumwa kwa shule za msingi huku shilingi bilioni kumi na nne zikitumwa kwa shule za upili ili kufanikisha shughuli za elimu.