WALIMU WA JSS WATISHIA KUSAMBARATAISHA SHUGHULI ZA MASOMO JANUARI IWAPO HAWATAAJIRIWA KWA MKTABA WA KUDUMU.
Walimu wa shule za sekondari ya msingi JSS katika katika kaunti ya Pokot magharibi wametishia kwamba watagoma kuanzia januari mwaka ujao iwapo tume ya huduma kwa walimu TSC haitawaajiri kwa mkataba wa kudumu.
Wakizungumza baada ya kuandaa maandamano mjini Makutano katika kaunti hiyo, walimu hao walipinga mpango wa TSC kuendelea kuwaajiri kwa kandarasi ya muda, wakilalamikia malipo duni na mazingira mabovu ya kufanyia kazi.
Wakati uo huo walimu hao walitaka shule za sekondari ya msingi kuondelewa katika kitengo cha shule za msingi na badala yake kujumuishwa na zile za upili, ikizingatiwa mazingira duni katika shule za msingi ambayo yanafanya vigumu kutekeleza majukumu yao kulingana na mtaala mpya wa elimu CBC.
“Sisi kama walimu wa JSS tunataka kuajiriwa kwa mktaba wa kudumu. Kama hilo halitatekelezwa, tutavuruga mipango ya masomo katika shule hizo, na hatutaenda darasani hadi matakwa yetu yatakaposikilizwa.” Walisema walimu.
Kauli ya walimu hao ilikaririwa na chama cha walimu wa shule za upili na vyuo vya kadri KUPPET tawi la Pokot magharibi chini ya mwenyekiti Joel Todokori na katibu mkuu Alfred Kamuto, ambao walisema ni kinyume cha sheria za leba kwa walimu hao kuhudumu tena kwa kandarasi ya mwaka mmoja.
“Hawa walimu wa JSS pia ni wakenya. Na tunavyojua, gharama ya maisha nchini imepanda sana na sasa mishahara yao iko chini. Tunataka TSC kuwaajiri walimu hawa kwa mkataba wa kudumu na kuongeza mishahara yao ili pia waweze kuishi maisha bora.” Walisema.
Tayari TSC imekariri msimamo wake kwamba itawapa walimu hao kandarasi ya mwaka mmoja zaidi kuanzia mwezi januari kinyume na matakwa yao.