WALIMU KUTOKA POKOT MAGHARIBI WANAOFUNZA TRANS NZOIA WAAPA KUTOREJEA DARASANI IWAPO HAWATAPEWA UHAMISHO.
Walimu kutoka kaunti ya Pokot magharibi wanaofunza katika shule za kaunti ya Trans nzoia waliandamana katika afisi za tume ya huduma kwa walimu TSC mjini Kapenguria kushinikiza kupewa uhamisho ili warejee kufunza katika kaunti hii.
Wakiongozwa na JK Riong’on walimu hao walisema kwamba juhudi zao kuishinikiza tume hiyo katika kaunti ya Trans nzoia kuwahamishia Pokot magharibi zimeonekana kufeli hatua iliyowafanya kuwasilisha matakwa yao kwa tume hiyo katika kaunti hiyo ya Pokot magharibi.
Waliitaka tume ya TSC kaunti hiyo kutokubali kuidhinisha majina ya walimu wasio wakazi, wakiapa kutorejea darasani iwapo matakwa yao hayatatiliwa maanani.
“Sisi haturudi darasani iwapo TSC haitatusikiliza. Tumetuma maombi kwa afisi za TSC kaunti ya Trans nzoia kutaka kurudi kufunza nyumbani lakini afisi hiyo imetupuuza. Na ndio sasa tunasema lazima watusikilize. Tunataka afisi ya TSC kaunti hii ya Pokot magharibi kutoidhinisha majina ya watu ambao wamehamishiwa kaunti hii na ambao si wakazi wa hapa.” Walisema walimu hao.
Walimu hao walisema kwamba wanapitia hali ngumu kutekelezea shughuli zao nje ya kaunti hiyo, wakidai kupitia unyanyapaa mikononi mwa wakazi wa maeneo wanakohudumu kwa kuhusishwa na visa vya wizi wa mifugo ambavyo ndicho chanzo kikuu cha utovu wa usalama katika kaunti zinazopatikana bonde la kerio.
“Tunanyanyaswa sana sisi. Tunafanya kazi lakini hatupandishwi hata vyeo. Sehemu ambazo tunafanyia kazi tunaonyeshwa unyanyapaa kwa kuitwa wezi wa mifugo. Hii ndiyo sababu tunataka turejee nyumbani, hatuwezi kuendelea kufanya kazi kwa njia hii.” Walisema.
Wakati uo huo walimu hao walidai kuwa ndoa zao nyingi zimevunjika kutokana na hali kwamba wanahudumu mbali na jamii zao.
“Wenzetu wengi ndoa zimevunjika kutokana na sera hii ya uhamisho wa walimu kuhudumu mbali na nyumbani kwao. Wengi sasa wamesalia bila waume na wake. Na hivyo tunaomba TSC waturudishe tu nyumbani tuwe karibu na jamii zetu.” Walisema.