WALIMU KUTOKA POKOT MAGHARIBI WALALAMIKIA KUNYIMWA UHAMISHO NA AFISI ZA TSC TRANS NZOIA.

Mamia ya walimu kutoka kaunti ya Pokot magharibi wameendelea kupiga kambi katika afisi ya Kamishna wa kaunti ya Trans-Nzoia,  kulalamikia hatua ya tume ya kuajiri walimu nchini, TSC,  kuchelewesha uhamisho wao kurejea katika shule zilizoko kaunti zao.

Mwaka uliopita bunge la kitaifa kupitia kamati ya elimu liliagiza tume ya kuajiri walimu nchini TSC kubadili uamuzi wa walimu kutofanyia kazi katika maeneo walikozaliwa na kukubalia maombi ya zaidi ya walimu alfu 14 waliokuwa wamehamishwa kurejea katika kaunti zao.

Mamia ya walimu kutoka Pokot magharibi walifika katika afisi za TSC kaunti ya Trans-Nzoia na afisi za kamishina, wakidai kuwa hawajafaidi agizo hilo.

“Walimu tunaofunza katika kaunti hii ya Trans nzoia kutoka Pokot magharibi tumenyimwa fursa ya kurejea kufunza nyumbani licha ya agizo kwamba walimu wanaofunza kaunti zingine warejee kaunti za nyumbani. Tumetuma maombi lakini hadi kufikia sasa hamna majibu yoyote.” Walisema.

Walisema walitarajia kujiunga na familia zao, na pia kupunguza uhaba wa walimu unaokabili kaunti ya pokot magharibi  baada ya walimu wengi kuondoka. 

“Kwa kipindi kirefu kumekuwa na upungufu wa walimu katika kaunti yetu ya Pokot magharibi na agizo la kuwataka walimu warejee katika kaunti zao lilikuwa limetupa matumaini ya angalau kutoa huduma zetu kwa kaunti yetu, lakini sasa ni kama tumenyimwa fursa hiyo.” Walisema.

Kwa wakati mmoja walimu hao waliandamana wakiungana na viongozi wao kuishinikiza serikali kuwapa uhamisho kurejea kufunza nyumbani.