WALEMAVU KAUNTI YA POKOT WATAKA HAKI KUTENDEKA
Walemavu katika kaunti hii ya Pokot magharibi wamelalamikia jinsi ambavyo liliendeshwa zoezi la uteuzi miongoni mwa vyama vya kisiasa wakidai kutengwa katika uteuzi huo licha ya kutuma maombi.
Wakiongozwa na mwenyekiti wa watu wanaoishi na ulemavu kaunti hii Moses Lomanat, watu hao wameisuta tume ya uchaguzi na mipaka nchini IEBC kwa kuwaacha nje katika orodhailiyochapishwa ya walioteuliwa licha ya sheria kuwa wazi kuhusu uteuzi huo.
Lomanat ametoa wito kwa vyama vya kisiasa kuzingatia sheria inayoruhusu nafasi mbili kutengewa watu wanaoishi na ulemavu.
Lomanat amesema kuwa watatetea haki yao na huenda wakalazimika kuandamana kulalamikia hatua hiyo huku pia akitoa wito kwa mashirika ya kijamii kuingilia kati na kuungana nao katika kushinikiza walemavu kutendewa haki.