WAKUU WA VYAMA VYA WALIMU WA WALALAMIKIA UCHACHE WA WALIMU POKOT MAGHARIBI.

Serikali ya kitaifa imetakiwa kuhakikisha kwamba inaajiri walimu wa kutosha wa shule za upili ili kukidhi idadi kubwa ya wanafunzi wanaotarajiwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka ujao hasa ikizingatiwa wanafunzi wa kwanza chini ya mtaala wa CBC watakuwa wakijiuga na shule za upili daraja la chini.

Katibu wa chama cha walimu wa shule za upili na vyuo vya Kadri KUPPET tawi la kaunti hii ya Pokot magharibi Alfred Kamutu alisema kwamba kaunti hii inakabiliwa na changamoto kubwa ya uchache wa walimu pamoja na madarasa ya kutosha.

“Kaunti hii ya Pokot magharibi ina changamoto kubwa hasaa upande wa walimu na madarasa. Ningependa serikali kutoa fedha za ujenzi wa madarasa na pia kuwaajiri walimu zaidi ili masomo yaendelee kwa njia nzuri.” Alisema Kamutu.

Aidha Kamutu aliitaka serikali kuangazia mazingira magumu ambayo walimu katika kaunti hii wanaendesha shughuli zao na kuhakikisha kwamba inawalipa marupurupu ya kufanyia kazi katika mazingira haya.

Aliitaka pia serikali kuwapandisha vyeo wasimamizi zaidi wa elimu.

“Walimu katika kaunti hii wanafanyia kazi katika mazingira magumu. Ningependa serikali kuwapa walimu marupurupu ya kufanyia kazi katika mazingira magumu na pia iwapandishe vyeo wale wasimamizi wa elimu.” Alisema.

Wakati uo huo Kamutu ametumia fursa hiyo kuwasihi wakuu wa shule za upili kuzingatia muda uliosalia kabla ya kuanza rasmi mtihani wa kitaifa na kutowatuma wanafunzi kila mara nyumbani kutafuta karo.

“Muda uliosalia kabla ya mtihani ni mchache sana na wakati huu si wa kuwatuma wanafunzi hasa wa kidato cha nne nyumbani kutafuta karo. Wanafunzi wanafaa kusalia shuleni kujiandaa kwa mitihani na kisha maswala ya karo yaangaliwe baadaye.” Alisema.

[wp_radio_player]