WAKUU WA SHULE WAPINGA MADAI YA KUHUSIKA UDANGANYIFU KATIKA MTIHANI WA KCSE MWAKA 2022.


Siku moja tu baada ya aliyekuwa seneta wa kaunti hii ya Pokot magharibi Samwel Poghisio kutaka uchunguzi kufanyiwa matokeo ya mtihani wa kitaifa kwa kidato cha nne KCSE mwaka 2022 kufuatia madai ya uwezekano wa watahiniwa kushiriki udanganyifu, baadhi ya wakuu wa shule kaunti hiyo wamepinga kuhusika tabia hiyo.
Naibu mwalimu mkuu wa shule ya upili ya wasichana ya Nasokol Dina Mnagat alitetea matokeo ambayo wanafunzi wa shule hiyo walipata akisema kwamba shule hiyo hairuhusu udanganyifu katika mitihani bali inaamini katika juhudi za mwanafunzi kupata alama anazostahili.
“Hamna wizi wa mitihani katika shule ya Nasokol na hatuwezi kuruhusu hilo, kwa sababu tunafahamu kwamba maisha ya baadaye ya mwanafuzi yataharibika anapohusika udanganyifu. Hatuwezi kuwafunza na kisha tuwafanyie mitihani na kuwaruhusu kwenda vyuo vikuu na matokeo yetu.” Alisema Mnagat.
Ni kauli ambayo ilitiliwa mkazo na mkurugenzi wa masomo katika shule hiyo Sevily Mwailemi ambaye alisema kwamba si wanafunzi wote waliofanya mtihani huo katika shule hiyo waliofanya vyema kwani wapo wanafunzi ambao walipata gredi za chini zaidi ishara kuwa hakukuwa na udanganyifu wowote.
“Mahali ambako kitu kizuri kipo ni lazima kuwe na watu wenye mawazo tofauti. Ila mimi nawahakikishia kwamba matokeo ambayo tulipata hapa ni ya haki na kupitia juhudi za wanafunzi wenyewe. Kwa sababu iwapo kungekuwa na udanganyifu hatungekuwa na gredi za chini sana ambazo baadhi ya wanafunzi walipata.” Alisema Mwailemi.
Shule hiyo ya Nasokol ilipata alama ya jumla ya 6.19417 katika mtihani wa KCSE mwaka 2022, matokeo ambayo wakuu wa shule hiyo walielezea kuridhishwa nayo baada ya kuimarika kutoka 5.343 ya mwaka 2021.