WAKUU WA SHULE POKOT MAGHARIBI WATAKIWA KUBUNI MBINU ZA KUIMARISHA MATOKEO YA MITIHANI YA KITAIFA.

Wakuu wa shule za kaunti ya Pokot magharibi pamoja na wadau wengine wametakiwa kuhakikisha kwamba wanaweka mikakati bora itakayosaidia kuhakikisha matokeo ya mitihani ya kitaifa yanaimarika hata zaidi.
Akizungumza katika shule ya upili ya ELCK Emboasis wakati wa kusherehekea matokeo bora ya mtihani wa kitaifa KCSE ya mwaka jana, naibu gavana wa kaunti Robert Komole alisema serikali ya kaunti imewekeza fedha nyingi katika sekta ya elimu na ni jukumu la wakuu hao kuhakikisha matokeo yanaimarika.
Komole alitumia fursa hiyo kuwahakikishia wazazi kwamba serikali ya gavana Simon Kachapin itatoa fedha za basari zilizosalia kuhakikisha kila mwanafunzi anapata shilingi alfu 25 kama karo jinsi alivyoahidi wakati wa kampeni.
“Nawahimiza walimu kwamba itakuwa vizuri kuinua shule zetu kuhakikishga kwamba matokeo yanaimarika. Sisi kama serikali ya kaunti tunatekeleza wajibu wetu wa kutoa fedha hasa za basari kuhakikisha shughuli zinaendelea shuleni inavyopasa.” Alisema Komole.
Aidha Komole alitoa wito kwa walimu wakuu kutokuwa wepesi wa kuwatuma nyumbani wanafunzi kutafuta karo na badala yake kutumia njia mbadala ya kuhakikisha karo hiyo inalipwa huku wanafunzi wakiendelea na masomo.
“Nawarai walimu wakuu kwamba wasiwe wepesi wa kuwatuma nyumbani wanafunzi kwa ukosefu wa karo bali watafute mbinu mbadala ya kuhakikisha karo inalipwa wakati wanafunzi wakiendeleza masomo.” Alisema.