WAKULIMA WATAKIWA KUJISALI KATIKA MAKUNDI YATAKAYOWAWEZESHA KUJIIMARISHA.

Wito umetolewa kwa wakulima katika kaunti hii ya Pokot magharibi kujiunga na mashirika mbali mbali yatakayowawezesha kuhifadhi fedha zao kwa manufaa ya shughuli zao hasa katika kutekeleza miradi mbali mbali ya kilimo.

Ni wito ambao umetolewa na mshirikishi wa mradi wa Kenya Climate Smart katika kaunti hii ya Pokot magharibi Philip Ting’aa ambaye amesema kwamba hatua hii itawawezesha wakulima kufanikisha kilimo chao kwa kuchukua mikopo kutoka kwa mashirika hayo kwa urahisi.

“Wakulima wajiunge na mashirika ambayo yatawasaidia kuweka fedha zao ambapo baadaye wataweza kuchukua mikopo kwa urahisi itakayowasaidia kuendeleza miradi yao ya kilimo.” Alisema Ting’aa.

Aidha Ting’aa alisema kwamba mashirika haya yatawawezesha wakulima kutekeleza miradi mbali mbali ambapo kiwango cha miradi hiyo kitategemea kiwango cha fedha ambazo wakulima wamekusanya kupitia kwa mashirika yao.

“Wanachama wa shirika wakiweka fedha zao wataweza kutekeleza miradi kulingana na kiwango cha fedha ambacho wamewekeza. Iwapo ni milioni moja watatekeleza mradi unaotoshana na fedha hizo. Hivyo inategemea kiwango wanachowekeza.” Alisema.

Wakati uo huo Ting’aa aliyataka makundi ya wakulima kukumbatia mfumo wa dijitali katika shughuli zao za kifedha ikiwemo kuhifadhi pesa katika akaunti zao pamoja na kutazama masalio kwenye akaunti hatua anayosema kwamba itahakikisha uwazi katika matumizi ya fedha.

“Katika dunia ya sasa shughuli nyingi hutekelezwa kidijitali. Tunawaomba wakuli ma wakumbatie mfumo huo katika kutekeleza shughuli zao za kifedha ikiwemo kuweka fedha kwenye akaunti pamoja na kuangalia masalio. Mfumo huu unasaidia katika kuhakikisha uwazi kwenye matumizi ya fedha.” Alisema.