WAKULIMA WALALAMIKIA KUJIKOKOTA SHUGHULI YA KUSAMBAZA MBOLEA KATIKA MAGHALA YA NCPB.

Wakulima katika kaunti ya Pokot magharibi wametaka kuharakishwa shughuli ya kutoa mbolea inayoendelea katika maghala ya NCPB.

Wakiongozwa na Harison Loyatum wakulima hao walisema kwamba mbolea ni kidogo mno katika maghala hayo hali inayofanya foleni ndefu kushuhudiwa kufuatia uchache wa malori ambayo yanaleta bidhaa hiyo.

Aidha wakulima hao waliitaka serikali kupunguza hata zaidi mbolea hiyo ilivyoahidi wakidai wapo wengi wa wakulima ambao hawawezi kumudu bei ya sasa licha ya kupunguzwa ikilinganishwa na ya msimu uliopita.

“Mbolea ni kidogo kwenye maghala ya NCPB kaunti hii. Lori tatu ambazo zinaleta mbolea hapa hazitoshi wananchi. Tumepiga foleni hapa kwa muda sasa na shughuli hii inaende polepole sana. Hivyo tungependa kuomba serikali kuongeza malori ambayo yanaleta mbolea hii ili kuharakisha shughuli.” Alisema Loyatum.

Wakati uo huo wakulima hao waliitaka serikali ya kaunti ya Pokot magharibi kuendeleza mpango wa kutoa mbegu kwa wakulima ili kujiandaa kwa ajili ya msimu wa upanzi unaotarajiwa hivi karibuni.

“Tunaomba hata serikali ya kaunti kuanza huo mpango wa kutoa mbegu kwa wananchi kwa sababu watu wengi sasa hawana pesa za kununulia mbegu wakati huu ambapo msimu wa upanzi umekaribia.” Alisema.

[wp_radio_player]