WAKULIMA WA ZAO LA MAHINDI WASHABIKIA HATUA YA SERIKALI KUSITISHA MIPANGO YA KUAGIZA MAHINDI KUTOKA NJE YA NCHI.

Wakulima na viongozi kaskazini mwa bonde la ufa wamesifia hatua ya serikali kusitisha uagizaji wa mahindi kutoka mataifa ya kigeni wakisema hatua hiyo itawapa fursa ya kuuza mahindi yao kwa bei ya kuridhisha.

Wakiongozwa na aliyekuwa gavana wa kaunti ya Pokot magharibi John Lonyangapuo na ambaye ni mmoja wa wakulima tajika eneo hilo wakulima hawa sasa wanaitaka serikali kuweka mikakati ya kuhakikisha pembejeo za bei nafuu zinawasili nchini kwa wakati unaofaa katika matayarisho ya msimu ujao wa upanzi.

“Tunaipongeza serikali kwa kubadili nia ya kuagiza mahindi kutoka mataifa ya nje na badala yake kutangaza kwamba mkulima wa hapa nchini ndiye atakayepewa kipau mbele. Hali hii itatuwezesha sasa kama wakulima kuuza mazao yetu kwa bei nzuri. Tunachotaka sasa ni kwa serikali kuleta pembejeo mapema ili wakulima wajiandae kwa msimu ujao wa upanzi.” Alisema Lonyangapuo.

Wakati uo huo Lonyangapuyo alipinga vikali mipango ya kuagiza vyakula vinavyokuzwa kijenetiki GMO akisema kwamba mbegu za vyakula vinavyokuzwa humu nchini zina uwezo wa kuzalisha vyakula vya kutosha kwa taifa.

Aidha alipendekeza kutoa elimu ya kutosha kwa wananchi iwapo serikali itahitaji kuzindua aina mpya ya mbegu za vyakula humu nchini kabla ya kuagizwa kwa matumizi ya wananchi.

“Tuna mbegu za hali ya juu hapa nchini na serikali inapasa kuwapa nafasi wakulima wa hapa nchini kukuza vyakula kwa kutumia mbegu zinazokuzwa nchini. Tuna uwezo wa kuzalisha chakula cha kutosha iwapo tutapewa nafasi hiyo. Iwapo serikali inataka kuingiza mbegu mpya nchini basi inafaa kuwahusisha kikamilifu wakulima na wananchi kwa jumla.” Alisema.

[wp_radio_player]