WAKULIMA TRANS NZOIA WAPIGWA JEKI KUFUATIA UVUMBUZI WA MTAMBO WA KUKAUSHA MAHINDI.

Na Benson Aswani
Chuo kikuu cha Moi kimezinduaTeknolojia mpya kupitia kwa mtambo wa kukausha na kuhifadhi nafaka katika juhudi za kuboresha mbinu ya kulinda mazao ya kilimo dhidi ya uharibifu hasa zao la mahindi mbali na kukabiliana na sumu ya aflatoxins ambayo imebainika kusababisha saratani ya ini.
Kwa mujibu wa mvumbuzi wa mtambo huo Dkt Isaiah Muchilwa mtambo huo una uwezo wa kukausha mahindi chini ya wiki mbili, hivyo kusadia kumpunguzia mkulima uharibifu wa nafaka mbali na kuimarisha ubora wa vyakula nchini, jambo ambalo afisa mkuu wa kilimo Kaunti ya Trans Nzoia Robert Musikoyo amesema wizara yake itaipa kipau mbele ili kupunguza uharibifu wanafaka kwa mkulima kutokana na unyevu.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa bodi ya chuo kikuu cha Moi Dkt Humphrey Kimani Njuguna amesema uvumbuzi huo utapiga jeki ajenda kuu ya serikali ya utoshelezaji wa chakula mbali na kukabili saratani ya ini inayotokana na nafaka iliyohifadhiwa kwenye unyevu.
Naye Naibu chansela wa chuo hicho Prof Isaac Koskei amesema uvumbuzi huo ni moja wapo ya mafunzo yanayokuzwa katika chuo hicho kuboresha hali ya maisha kwa kutumia vifaa na vijana wa humu nchini.