WAKULIMA POKOT MAGHARIBI WATAKIWA KUJIUNGA KWENYE MAKUNDI ILI KUNUFAIKA NA HUDUMA MBALI MBALI.

Meneja wa shirika la E for Impact moja ya mashirika ambayo yanaendeleza miradi mbali mbali ya kuwawezesha wakulima kaunti ya Pokot magharibi Banadet Mutinda ametoa wito kwa wakulima katika kaunti hiyo kujiunga katika makundi ambayo yatawasaidia kutekeleza shughuli zao kwa njia bora.

Akizungumza eneo la Muino wakati alipokutana na wakulima wa shirika la muino, akiandamana na maafisa kutoka shirika la NRT, Mutinda alisema wakulima wataweza kunufaika pakubwa iwapo watajiunga katika makundi kwani yatawawezesha kuwa na sauti.

“Mkulima akiwa pekee kuendeleza shughuli zake mwenyewe hataweza kuwa na nguvu au sauti jinsi ambavyo ingekuwa iwapo angukuwa kwenye kikundi. Haya makundi yanasaidia sana wakulima kusikika na kupata pembejeo na hata katika kutafuta soko kwa ajili ya mazao yao.” Alisema Mutinda.

Ni kauli ambayo ilisisitizwa na afisa katika shirika la NRT Alois Naitira ambaye alisema lengo lao kuu ni kuhakikisha hali ya maisha ya jamii inaimarika huku akipongeza serikali ya kaunti kupitia idara mbali mbali kwa ushirikiano ambao inatoa kwa mashirika ya kijamii.

“Tumeshirikiana na mashirika mbali mbali lengo letu kuu likiwa kuhakikisha kwamba kupitia shughuli za kilimo na miradi mingine, hali ya maisha ya mkazi wa kaunti hii inaimarika. Nashukuri pia serikali ya kaunti kwa kushirikiana vyema nasi na hata kutupa mazingira bora ya kutekeleza shughuli zetu kuhakikisha mkulima anapata huduma zinazostahili.” Alisema Naitira.