WAKULIMA POKOT MAGHARIBI WAKADIRIA HASARA KUFUATIA UVAMIZI WA VIWAVI JESHI.

Serikali ya kaunti hii ya Pokot magharibi inaendelea kuweka mikakati ya kukabili kusambaa kwa viwavi jeshi ambao wameripotiwa kuvamia mashamba ya wakulima katika maeneo mbali mbali ya kaunti hii wakati huu ambapo wakulima wengi wamepanda mimea yao.
Akizungumza na kituo hiki afisa mkuu katika wizara ya kilimo kaunti hii Samson Nyangaluk amesema kuwa tayari serikali ya kaunti imeagiza dawa ya kutosha ya kunyunyizia mashamba ambayo tayari yameathirika na uvamizi wa wadudu hao hatari ili kuzuia uharibifu zaidi.
Nyangaluk amesema kuwa maafisa kutoka wizara hiyo watatumika katika zoezi hilo la kunyunyizia dawa pamoja kuwashauri wakulima sehemu za kununua na jinsi ya kutumia dawa hiyo akitoa wito kwa wakulima kutoa ushirikiano mwema kwa maafisa hao ili kuhakikisha wadudu hao wanakabiliwa.
Wakati uo huo Nyangaluk amewataka wakulima wanaoshuhudia wadudu hao kwenye mashamba yao kutoa taarifa mapema kwa maafisa husika ili kuwakabili mapema kabla ya kuenea ikizingatiwa wadudu hao wanaenea kwa kasi sana.