WAKULIMA POKOT MAGHARIBI WAHIMIZWA KUZAMIA KILIMO CHA NYASI.
Na Benson Aswani.
Serikali ya kaunti hii ya Pokot magharibi kupitia wizara ya kilimo inalenga kuimarisha kilimo cha nyasi hasa katika kipande cha ardhi cha Nasukuta ili kutosheleza mahitaji ya wakulima wa mifugo kaunti hii.
Akizungumza wakati wa kuwapokea wafadhili wa kuweka ua kwenye ardhi hiyo ya Nasukuta ili kuhifadhi nyasi, waziri wa kilimo na mifugo kaunti hiyo Wilfred Longronyang alisema lengo kuu la serikali ni kuhakikisha kwamba wafugaji hawahangaiki kutafuta lishe.
Aidha Longronyang alitoa wito kwa wakulima katika kaunti ya Pokot magharibi kuzamia kilimo cha nyasi ili kuwe na lishe ya mifugo ya kutosha.
“Sisi kama serikali tukiongozwa na gavana wetu tuna lengo kubwa katika shamba hili la kuhakikisha linajisimamia na kutoa lishe ya kutosha kwa wafugaji. Nawahimiza wakulima kuiga mfano huu wa kufunga mashamba na kupanda nyasi. Kilimo cha nyasi si ngumu ni rahisi sana.” Alisema Longronyang.
Afisa kutoka baraza la maendeleo kwenye kaunti kame FCDC Adan Vule ambaye anaendeleza shughuli hiyo, alisema hatua hii itasaidia katika kuhakikisha uzalishaji wa hali ya juu wa lishe ya mifugo na pia kukabili athari za hali ya ukame.
“FCDC inashirikiana na serikali ya kaunti ya Pokot magharibi kuhakikisha kwamba tunaimarisha uzalishaji wa lishe ya mifugo, na kwamba mpango huu pia unasambazwa maeneo mengi ya kaunti hii, ili kuwahakikishia wakulima usalama kutokana na ukame.” Alisema Vule.