Wakulima Pokot magharibi wahimizwa kuanza upanzi

Shamba ambalo Linatayarishwa kwa Upanzi Wa mahindi,picha/Maktaba
Na Benson Aswani,
Idara ya kilimo katika kaunti ya Pokot magharibi imetoa wito kwa wakulima kuanza shughuli ya upanzi wakati huu ambapo kumeendelea kushuhudiwa mvua sehemu mbali mbali za kaunti hiyo na maeneo mengine ya nchi.
Akizungumza na kituo hiki jumatano, mkurugenzi katika idara hiyo Philip Ting’aa alielezea umuhimu wa kupanda mapema katika siku za mwanzo za msimu wa mvua, akisema kwamba mahindi yanayopandwa mapema huwa na mazingira bora ya kufanya vyema.
“Wakati huu ambapo mvua imeanza nawahimiza tu wakulima katika kaunti hii kwamba ni bora zaidi kupanda mapema kwa sababu mahindi yanayopandwa mapema huwa na nafasi bora ya kufanya vyema kutokana na joto ambalo lipo kwenye mchanga,” alisema Ting’aa
Aidha Ting’aa aliwataka wakulima ambao ndio mwanzo wanaandaa mashamba yao kujizuia na kuchoma masalio yaliyo katika mashamba yao kwani hatua hiyo inaharibu rutuba ya mchanga, hali ambayo itaathiri ukuaji wa mimea.
“Naomba kwamba wakulima wasichome masalio katika mashamba yao katika maandalizi ya msimu wa upanzi kwa kuwa hatua hiyo inaharibu rutuba kwenye mchanga,” alisema.
Wakati uo huo Ting’aa aliwahakikishia wakulima kutoka nyanda za juu katika kaunti hii kwamba zipo mbegu za kutosha ambazo zinafaa mazingira ya maeneo hayo.
“Wakati huu tuna mbegu za kutosha hasa kwa wakulima wa nyanda za juu na najua kwamba wakulima wanaelewa aina ya mbegu ambazo zinafaa mazingira hayo,” alisema.