WAKULIMA POKOT MAGHARIBI WAENDELEA KUNUFAIKA KUPITIA SHUGHULI ZA KENYA CLIMATE SMART AGRICULTURE.

Serikali ya kaunti ya Pokot magharibi kwa ushirikiano na ya kitaifa kupitia mradi wa Kenya climate smart pamoja na benki ya dunia, imeendeleza miradi mbali mbali katika kaunti hiiyo kwa lengo la kuwanufaisha wakazi hasa wanaojihusisha na kilimo cha ufugaji.

Hii ni baada ya mradi huo kufadhili shirika la Tulwet co-operative society linalojishughulisha na kutengeneza bidhaa zinazotokana na maziwa pamoja na vyakula vya mifugo, uongozi wa shirika hilo ukisema hatua hiyo itasaidia pakubwa kupanua shughuli zake.

 “Tumepata ufadhili kutoka kwa serikali kupitia mradi wa Kenya climate smart agriculture ambao utatusaidia kununua mitambo ya kutengeneza chakula cha mifugo na kupanua zaidi hili shirika. Hatua hiyo pia itasaidia kubuni nafasi za ajira pindi tu mitambo hii itakapoanza kufanya kazi.” Alisema Jackson Peter meneja wa shirika hilo.

Afisa katika mradi wa Kenya climate smart carolyne Misiko alisema kwamba lengo kuu la mradi huo ni kuhakikisha kwamba shughuli za wakulima zinaimarika na mkulima anapata faida kutokana na shughuli za kilimo anazojihusisha nazo.

“Lengo letu kuu kama mradi ni kuhakikisha kwamba kilimo kimeimarika kwa hali ambayto itaimarisha mapato kwa wakulima. Pia tunahakikisha kwamba mkulima anainuka baada ya kupitia changamoto mbali mbali kama vile athari za ukame.” Alisema Misiko.

Wanachama wa shirika hilo walielezea kunufaika pakubwa, wakisema shirika hilo limewapelekea kutambua umuhimu wa kilimo hasa cha ng’ombe wa maziwa kwani awali walikuwa wakikadiria hasara kubwa kwa kukosa soko la maziwa yao kufuatia soko kufurika bidhaa hiyo.

Shirika hili limetufaa sana sisi kama wakulima kwa sababu kabla ya kufunguliwa tulikuwa tukipitia hasara kubwa sana katika shughuli zetu kwa sababu wakati mwingine tulikuwa tukikosa sehemu ya kuuza maziwa kutokana na kufurika bidhaa hiyo sokoni. Lakini sasa tunafurahia kwa sababu tuna sehemu ya kupeleka maziwa yetu.” Walisema.