WAKENYA WAINGIA DEBENI HUKU IDARA YA POLISI IKIWAHAKIKISHIA USALAMA.


Wakazi wa kaunti hii ya Pokot magharibi wanapoendelea kujitokeza katika shughuli ya upigaji kura idara ya polisi kaunti hii imetoa wito kwa wote wanaoshiriki zoezi hilo kuhakikisha kuwa wanarejea makwao punde tu wanapopiga kura zao.
Kamanda wa polisi kaunti hii Peter Katam amesema kuwa polisi hawataruhusu mikusanyiko ya watu katika vituo vya kupigia kura ikizingatia vituo vingi vinavyotumika ni shule na ni jukumu lao kuhakikisha kuwa mali ya shule inalindwa dhidi ya uharibifu wowote.
Wakati uo huo Katam amewataka wakazi kukubali matokeo ya uchaguzi huo na kutojihusisha na vitendo vyovyote ambavyo huenda vikavuruga hali ya usalama katika kaunti hii.
Aidha Katam amewahakikishia wakazi wa kaunti hii kwamba hali ya usalama imeimarishwa na kuwataka kutokuwa na hofu yoyote wakati wanapohusika shughuli hii muhimu ya upigaji kura hasa katika maeneo ya mipakani.