WAKENYA WAHIMIZWA KUWA TAYARI KWA HALI NGUMU ZAIDI, SERIKALI YA RAIS RUTO IKISUTWA KWA KUWA NA NIA YA KUMKANDAMIZA MWANANCHI.

Tangazo la mamlaka ya kudhibiti kawi EPRA kwamba itaongeza bei ya bidhaa za mafuta ya petroli kufuatia hatua ya rais William Ruto kutia saini mswada wa fedha wa mwaka 2023, limeendelea kuibua hisia kali miongoni mwa wananchi.

Wakazi wa kaunti ya Pokot magharibi wameusuta uongozi wa rais William Ruto wakisema kwamba una nia ya kuwakandamiza zaidi wananchi wenye kipato cha chini kinyume kabisa na ahadi yake wakati wa kampeni.

Wakazi hao walisema kwamba idadi kubwa ya wakenya kwa sasa wanapitia hali ngumu kufuatia kupanda gharama ya maisha, na hatua ya rais Ruto kutia saini mswada wa fedha ambao unaenda kupandisha zaidi gharama ya maisha ni usaliti kwa wakenya waliompigia kura.

“Rais Ruto alituahidi kuhakikisha kwamba gharama ya maisha inarudi chini. Lakini sasa anavyofanya ni tofauti sana na jinsi alivyokuwa kisema wakati wa kampeni. Gharama ya maisha sasa imepanda kuliko serikali yoyote iliyowahi kuwa mamlakani, hadi watu tuliompigia kura tunaona kama tumesalitiwa.” Walisema.

Wakazi hao walisema wanaunga mkono hatua ambazo zinachukuliwa na kinara wa chama cha muungano wa azimio la umoja one Kenya Raila Odinga katika kushinikiza serikali kushughulikia gharama ya juu ya maisha, ikiwemo kuandaa maandamano, wakimtaka rais Ruto kubatilisha uamuzi wake.

“Sisi tunaunga mkono maandamano ambayo kinara wa azimio Raila Odinga anapanga tarehe saba july. Kwa sababu sasa yeye ameonekana kuwa kiongozi mwenye anatetea hali ya mwananchi. Na ni haki ya mwananchi kuandamana kulalamikia maswala ambayo hajaridhishwa nayo.” Walisema.

Katika taarifa kwa vyombo vya habari alhamisi, EPRA ilisema kwamba itatangaza ongezeko la bei ya mafuta kufuatia hatua ya rais William Ruto kuongeza maradufu kodi ya thamani ya ziada VAT kwa bidhaa za mafuta ya petroli kutoka asilimia 8 hadi asilimia 16.