WAKENYA KUENDELEA KUGHARAMIKIA HALI NGUMU YA MAISHA HADI BAADA YA UCHAGUZI MKUU.


Wakenya watalazimika kuendelea kugharamikia hali ngumu ya maisha inayotokana na kuendelea kuongezeka bei ya mafuta hadi baada ya uchaguzi mkuu wa tarehe 9 mwezi agosti wakati vikao vya bunge vitakaporejelewa baada ya kuchaguliwa viongozi wapya.
Haya ni kulingana na seneta wa kaunti hii ya Pokot magharibi Samwel Poghisio ambaye amesema kuwa kwa sasa bunge la seneti halina uwezo wa kujadili na kurekebisha hali hiyo kutokana na hali kuwa tayari bunge la kitaifa limeahirisha vikao vyake hadi baada ya uchaguzi mkuu ujao.
Poghisio ambaye pia ni kiongozi wa wengi katika bunge la seneti amesema kuwa vikao vya bunge hilo la seneti vitarejelewa leo kwa kujadili sheria ambazo zilifaa kukamilishwa kabla ya alhamisi juma jana ambapo vikao hivyo vilifaa kuahirishwa rasmi hadi baada ya uchaguzi wa mwezi agosti.
Amesema kuwa vikao vya bunge hilo sasa vitafungwa rasmi hii leo baada ya kupasishwa miswada yote iliyotarajiwa kupasishwa na kisha wabunge katika bunge hilo waage rasmi kabla ya vikao kuahirishwa.