WAKAZI WATAKIWA KUTOYAUZA MAZAO YAO YOTE WAKATI WA MAVUNO ILI KUKABILI BAA LA NJAA MSIMU WA UKAME.

Wito umetolewa kwa wakazi wa kaunti ya Pokot magharibi kuwa makini wakati wanapovuna mazao yao na kutoyauza yote ili kukabiliana na baa la njaa hasa misimu ya ukame.

Ni wito wake afisa wa miradi katika shirika la action against hunger Betty Cheyech ambaye alisema kwamba jamii nyingi katika kaunti hiyo hupitia wakati mgumu kufuatia ukosefu wa chakula nyakati za ukame hali aliyosema huenda inatokana na hatua ya wakazi kuuza mavuno yao yote.

“Wengi wa wakazi huuza mazao punde baada ya kuvuna. Hali hii hupelekea wengi kuhangaika wakati kunaposhuhudiwa ukame kwa sababu sasa hawana chakula kwa familia pamoja na mifugo. Ninawashauri wakulima kuwa makini na kutouza chakula chote wanapovuna.” Alisema Cheyech. 

Aidha Cheyech aliwataka wakazi ambao wengi wao ni wafugaji kutotegemea tu kilimo cha ufugaji na badala yake kuangazia pia kilimo cha mimea ili kuwa na chakula cha kutosha na kutoathirika zaidi wakati wa ukame.

“Ni wakati ambapo wakazi wa kaunti hii wanapasa kutotegemea mifugo pekee bali kupanda pia mimea, kwa sababu kunapotokea kipindi cha ukame,huwa vigumu kupata chakula cha mifugo na hivyo mifugo hao kuondokea kutokuwa na faida kwa wakazi.” Alisema.

Shirika hilo la action against hunger kwa ushirikiano na mashirika mengine yasiyo ya serikiali yanaendeleza miradi mbali mbali ya kuwafaa wakazi wa kaunti hii kutokana na ukame ambao umeathiri jamii nyingi.

[wp_radio_player]