WAKAZI WATAKA MAREKEBISHO KATIKA IDARA YA POLISI POKOT MAGHARIBI.

Wakazi katika kaunti hii ya Pokot magharibi wameendelea kushutumu kisa ambapo mwanamke mmoja alipigwa risasi jumatatu na afisa wa polisi katika soko la Kacheliba katika kile ambacho kinadaiwa kuwa mzozo uliohusu pesa.

Kulingana na wakazi waliokuwepo katika eneo la tukio, mzozo ulizuka baina ya mwanamke huyo na D.E.O wa Kongelai Moses Ekisa aliyekuwa ameandamana na polisi kwa jina Isaac Oshome aliyemfyatulia risasi mwanamke huyo aliyekuwa akimdai fedha zake wakazi wakitaka hatua kuchukiliwa.

“Huyu msichana alikuwa anadai mtu pesa yake sasa huyu jamaa akakasirika na kuanza kumgombeza. Tulipotoka nje tukapata jamaa amemkaba kabisa na mwishowe akampiga risasi. Tunaomba tu haki ifanyike kwa huyu mama.”´Walisema wakazi.

Wakazi hao sasa wanataka maafisa wa usalama ambao wamechukua muda mrefu katika vituo vya polisi katika kaunti hii ya Pokot magharibi kupewa uhamisho, wakidai wengi wao wanashirikiana na wakuu wao ili wasalie katika kaunti hii na kuwahangaisha wakazi.

“Hawa askari wanasumbua watu sana. Wanakamata watu hata saa moja tu jioni bora wamewapata barabarani. Wengine wao wamekaa hapa miaka mingi na hawapewi uhamisho. Ni kama wanashirikiana na wakubwa wao ili wasalie pokot magharibi kuwahangaisha wakazi.” Walisema.

OCPD wa Kapenguria Kipkemoi Kirui amelaani vikali kisa hicho na kuwataka maafisa wa polisi na maafisa wengine wa serikali wanaohudumu katika sekta ya usalama kutotumia vyeo vyao vibaya na badala yake kuwatumikia vyema wananchi.

“Tunalaani kabisa hili tukio na tunawahimiza maafisa wetu wa polisi kwamba wasiwe wanatumia silaha zao vibaya na pia maafisa wa serikali wasitumie polisi vibaya. Wanatakikana kuwa maafisa wa kuwahudumia vyema wananchi wala si kuwanyanyasa.” Alisema Kirui.

Wawili hao wamefikishwa jumanne kotini kufunguliwa mashitaka.